11 Hata itakuwa, siku zako zitakapotimia, uende na babazo, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayekuwa wa wana wako; nami nitaufanya imara ufalme wake.
12 Yeye ndiye atakayenijengea nyumba, nami nitakifanya imara kiti cha enzi cha ufalme wake milele.
13 Nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; wala sitamwondolea fadhili zangu, kama nilivyomwondolea yeye aliyekuwa kabla yako;
14 ila nitamstarehesha katika nyumba yangu na katika ufalme wangu milele; na kiti chake cha enzi kitathibitishwa milele.
15 Kwa maneno hayo yote, na kwa maono hayo yote, ndivyo Nathani alivyonena na Daudi.
16 Ndipo akaingia Daudi mfalme, akaketi mbele za BWANA; akasema Mimi ni nani, Ee BWANA Mungu, na nyumba yangu ni nini, hata umenileta hata hapa?
17 Tena jambo hili lilikuwa dogo machoni pako, Ee Mungu; hata umeleta habari ya nyumba yangu mimi, mtumwa wako, kwa miaka mingi inayokuja, nawe umeniangalia sawasawa na hali ya mtu mwenye cheo, Ee BWANA Mungu.