14 Lakini sasa ufalme wako hautadumu; BWANA amejitafutia mtu aupendezaye moyo wake, naye BWANA amemwamuru yeye kuwa mkuu juu ya watu wake, kwa sababu wewe hukulishika neno lile BWANA alilokuamuru.
15 Basi Samweli akaondoka, akapanda kutoka Gilgali mpaka Gibea ya Benyamini. Naye Sauli akawahesabu watu waliokuwapo pamoja naye, wapata kama mia sita.
16 Naye Sauli, na mwanawe Yonathani, na watu waliokuwapo pamoja nao, wakakaa huko Geba ya Benyamini; lakini Wafilisti wakatua katika Mikmashi.
17 Nao watekaji wa nyara wakatoka katika marago ya hao Wafilisti, vikosi vitatu; kikosi kimoja kikageukia njia iendayo Ofra, mpaka nchi ya Shuali;
18 na kikosi kingine kikageukia njia iendayo Beth-horoni; na kikosi kingine kikageukia njia ya mpakani ielekeayo bonde la Seboimu upande wa nyika.
19 Basi, hakuonekana mhunzi ye yote katika nchi yote ya Israeli; kwa kuwa Wafilisti walisema, Waebrania wasije wakajifanyizia panga au mikuki;
20 lakini Waisraeli wote hushuka kwa Wafilisti, ili kunoa kila mtu jembe lake, na mundu wake, na shoka lake, na sululu yake;