29 Ndipo Yonathani akasema, Babangu ameifadhaisha nchi; tafadhali, angalia jinsi macho yangu yalivyotiwa nuru, kwa sababu nalionja asali hii kidogo.
30 Je! Si zaidi sana, kama watu wangalikula na kushiba leo katika nyara hizi za adui zao walizoziteka? Kwa maana haukuwa uuaji mkuu sasa katikati ya Wafilisti.
31 Nao wakawapiga watu miongoni mwa Wafilisti siku ile kutoka Mikmashi mpaka Ayaloni; na hao watu walikuwa wamepungukiwa sana na nguvu.
32 Basi watu wakazirukia zile nyara, wakatwaa kondoo, na ng’ombe, na ndama, na kuwachinja papo hapo juu ya nchi, nao wale watu walikuwa wakiwala pamoja na damu.
33 Ndipo wakamwambia Sauli, wakisema, Angalia, watu hao wanakosa juu ya BWANA, kwa jinsi wanavyokula pamoja na damu. Naye akasema, Ninyi mmefanya kwa hiana; vingirisheni kwangu leo jiwe kubwa.
34 Kisha Sauli akasema, Haya! Tawanyikeni katikati ya watu mkawaambie, Nileteeni hapa kila mtu ng’ombe wake, na kila mtu kondoo wake, mkawachinje hapa na kula; wala msikose juu ya BWANA, kwa kula pamoja na damu. Nao watu wote wakaleta kila mtu ng’ombe wake pamoja naye usiku ule, nao wakawachinja hapo.
35 Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA.