12 Naye Yonathani akamwambia Daudi, BWANA, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili?
13 BWANA anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na BWANA awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14 Nawe utanionyesha fadhili za BWANA, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai;
15 lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule BWANA atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.
16 Basi Yonathani akafanya agano na jamaa yake Daudi, akisema, BWANA naye atayataka mkononi mwa adui zake Daudi.
17 Naye Yonathani akamwapisha Daudi mara ya pili, kwa ajili ya upendo aliokuwa nao kwake; kwa maana alimpenda kama alivyoipenda roho yake mwenyewe.
18 Kisha Yonathani akamwambia, Kesho ni mwandamo wa mwezi, nawe utakosekana, kwa sababu kiti chako kitakuwa hakina mtu.