9 Naye Yonathani akasema, Haya na yawe mbali nawe, kwa maana kama ningejua ya kuwa baba yangu amekusudia kukutenda neno baya, je! Singekuambia?
10 Basi Daudi akamwambia Yonathani, Ni nani atakayeniambia, ikiwa baba yako amekujibu maneno makali?
11 Yonathani akamwambia Daudi, Twende zetu nje mashambani. Wakatoka wote wawili, wakaenda mashambani.
12 Naye Yonathani akamwambia Daudi, BWANA, Mungu wa Israeli, na awe shahidi; nitakapokuwa nimekwisha kumwuliza baba yangu, kama wakati huu kesho, au siku ya tatu, angalia, kama liko neno jema la kumfaa Daudi, je! Nisikupelekee habari na kukufunulia neno hili?
13 BWANA anitende mimi, Yonathani, hivyo, na kuzidi, ikiwa yampendeza babangu kukutenda mabaya, nisipokufunulia haya, na kukupeleka uende zako kwa amani; na BWANA awe pamoja nawe, kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14 Nawe utanionyesha fadhili za BWANA, ili nisife, si wakati huu tu maadamu mimi ni hai;
15 lakini pamoja na hayo, hata jamaa yangu pia hutawaondolea kabisa fadhili zako; la, hata wakati ule BWANA atakapokuwa amewaondoa kabisa adui za Daudi wote pia katika uso wa nchi.