20 Naye Daudi akatwaa makundi yote ya kondoo na ng’ombe, ambao waliwatanguliza mbele ya wanyama wale wengine, wakasema, Hao ndio nyara za Daudi.
21 Kisha Daudi aliwafikilia wale watu mia mbili, waliokuwa wametaka kuzimia, hata wasiweze kumfuata Daudi, wale waliowaacha wakae karibu na kijito cha Besori; nao wakatoka nje ili kumlaki Daudi, na kuwalaki hao watu waliokuwa pamoja naye, naye Daudi alipowakaribia hao watu, aliwasalimu.
22 Ndipo watu waovu wote na wale wasiofaa, miongoni mwa hao waliokwenda pamoja na Daudi, wakasema, Kwa kuwa watu hawa hawakuenda pamoja na sisi, hatutawapa kitu cho chote katika hizo nyara tulizozitwaa tena, isipokuwa kila mtu atapewa mkewe na watoto wake, wawachukue na kwenda zao.
23 Ndipo Daudi akasema, La, ndugu zangu, msitende hivyo katika hizo nyara alizotupa BWANA, ambaye ndiye aliyetuhifadhi, akalitia mikononi mwetu lile jeshi lililokuja kinyume chetu.
24 Tena ni nani atakayewasikiliza ninyi katika jambo hili? Kwa kuwa kama lilivyo fungu lake yeye ashukaye vitani, ndivyo litakavyokuwa na fungu lake huyo akaaye karibu na vyombo; watagawiwa sawasawa.
25 Basi ikawa hivyo tangu siku ile na baadaye; akaiweka iwe amri na agizo la Israeli hata leo.
26 Basi Daudi alipofika Siklagi, aliwapelekea wazee wa Yuda, rafiki zake, sehemu ya nyara, akasema, Angalieni, zawadi yenu katika nyara za adui za BWANA;