7 Kisha Daudi akamwambia Abiathari, kuhani, mwana wa Ahimeleki, Tafadhali niletee hapa hiyo naivera. Naye Abiathari akamletea Daudi naivera huko.
8 Daudi akauliza kwa BWANA, akasema, Je! Nikiwafuata jeshi hili, nitawapata? Naye akamjibu, Fuata; kwa kuwa hakika utawapata, nawe hukosi utawapokonya wote.
9 Basi Daudi akaenda, yeye na wale watu mia sita waliokuwa pamoja naye, nao wakakifikilia kijito Besori, ambapo wale walioachwa nyuma walikaa.
10 Lakini Daudi akakaza kufuata, yeye na watu mia nne; kwa maana watu mia mbili walikaa nyuma, ambao walitaka kuzimia hata hawakuweza kukivuka hicho kijito Besori.
11 Nao wakamkuta Mmisri mavueni, wakamleta kwa Daudi, na kumpa chakula, naye akala; nao wakampa maji ya kunywa;
12 kisha wakampa kipande cha mkate wa tini, na vishada viwili vya zabibu; naye akiisha kula roho yake ikamrudia; kwa maana alikuwa hakula chakula wala kunywa maji, siku tatu mchana na usiku.
13 Ndipo Daudi akamwuliza, Wewe u mtu wa nani; nawe umetoka wapi? Naye akasema, Mimi ni kijana wa Misri, mtumwa wa Mwamaleki mmoja; bwana wangu aliniacha, kwa sababu tangu siku hizi tatu nalishikwa na ugonjwa.