5 Na sanduku la agano la BWANA lilipoingia kambini, Israeli wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma.
6 Nao Wafilisti waliposikia mshindo wa zile kelele, walisema, Maana yake nini mshindo wa kelele hizi kubwa katika kambi ya Waebrania? Wakatambua ya kuwa sanduku la BWANA limefika kambini.
7 Wafilisti wakaogopa, maana walisema, Mungu ameingia kambini. Wakasema, Ole wetu! Kwani halijawa jambo kama hili tangu hapo.
8 Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya kila namna jangwani.
9 Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume, mkapigane nao.
10 Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu.
11 Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa.