3 Basi Samweli akawaambia nyumba yote ya Israeli, akasema, Ikiwa mnamrudia BWANA kwa mioyo yenu yote, basi, iondoleeni mbali miungu migeni, nayo Maashtorethi yatoke kwenu, mkamtengenezee BWANA mioyo yenu, mkamtumikie yeye peke yake; naye atawaokoa katika mikono ya Wafilisti.
4 Ndipo wana wa Israeli wakayaondoa Mabaali na Maashtorethi, wakamtumikia BWANA peke yake.
5 Samweli akasema, Wakusanyeni Israeli wote Mispa, nami nitawaombea ninyi kwa BWANA.
6 Wakakusanyika huko Mispa, wakateka maji na kuyamimina mbele za BWANA; wakafunga siku ile, wakasema huko, Tumemfanyia BWANA dhambi. Samweli akawaamua wana wa Israeli huko Mispa.
7 Hata Wafilisti waliposikia ya kuwa wana wa Israeli wamekusanyika huko Mispa, mashehe wa Wafilisti walipanda juu ili kupigana na Israeli. Nao wana wa Israeli waliposikia, wakawaogopa Wafilisti.
8 Wana wa Israeli wakamwambia Samweli, Usiache kumlilia BWANA, Mungu wetu, kwa ajili yetu, kwamba atuokoe na mikono ya Wafilisti.
9 Ndipo Samweli akatwaa mwana-kondoo mchanga, akamtolea BWANA sadaka ya kuteketezwa nzima; Samweli akamlilia BWANA kwa ajili ya Israeli; BWANA akamwitikia.