1 Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu.
2 Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.
3 Na punda za Kishi, baba yake Sauli, walikuwa wamepotea. Kishi akamwambia Sauli mwanawe, Haya basi, twaa mtumishi mmoja pamoja nawe, uondoke, uende ukawatafute punda hao.
4 Naye akapita kati ya nchi ya milima milima ya Efraimu, akapita na kati ya nchi ya Shalisha, lakini hawakuwaona; kisha wakapita kati ya nchi ya Shaalimu, wala huko hawakuwako; wakapita kati ya nchi ya Wabenyamini, lakini hawakuwapata.
5 Hata walipofika nchi ya Sufu, Sauli akamwambia yule mtumishi aliyefuatana naye, Haya, na turudi, baba yangu asije akaacha kufikiri habari za punda akatufikiri sisi.
6 Naye akamwambia, Tazama, katika mji huu mna mtu wa Mungu, naye ni mtu mwenye kuheshimiwa; yote asemayo hutukia kweli kweli; basi, twende huko; labda yeye aweza kutuambia habari ya safari yetu tunayoiendea.