8 Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako,
9 ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.
10 Na tazama, nitawapa watumishi wako, wachongaji wakatao miti, kori ishirini elfu za ngano iliyopondwa, na kori ishirini elfu za shayiri, na bathi ishirini elfu za mvinyo na bathi ishirini elfu za mafuta.
11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akajibu kwa waraka, aliompelekea Sulemani, Ni kwa sababu BWANA awapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme juu yao.
12 Hiramu akasema tena, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, aliyezifanya mbingu na nchi, ambaye amempa mfalme Daudi mwana wa hekima, mwenye busara na akili, ili amjengee BWANA nyumba, na nyumba kwa ufalme wake.
13 Na sasa nimemtuma mtu mstadi, mwenye akili, yaani, Hiramu baba yangu,
14 mwana wa mwanamke wa binti za Dani, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, ajuaye sana kazi ya dhahabu, na ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya mawe, na ya mti, ya urujuani, ya samawi, na ya kitani safi, na ya nyekundu; tena mstadi wa kuchora machoro yo yote, na wa kufikiri fikira yo yote; apate kuagiziwa kazi pamoja na watu wako wastadi, tena na wastadi wa bwana wangu Daudi baba yako.