3 Mfalme akageuza uso wake, akawabarikia mkutano wote wa Israeli; na mkutano wote wa Israeli wakasimama.
4 Akasema, BWANA, Mungu wa Israeli, ahimidiwe, aliyenena kwa kinywa chake na baba yangu Daudi, akalitimiza kwa mikono yake, akasema,
5 Tangu siku ile nilipowatoa watu wangu katika nchi ya Misri, sikuchagua mji wo wote wa kabila zote za Israeli ili kujenga nyumba, jina langu liwe humo; wala sikumchagua mtu ye yote awe mkuu juu ya watu wangu Israeli;
6 lakini nimeuchagua Yerusalemu, jina langu liwe humo; na Daudi nimemchagua awe juu ya watu wangu Israeli.
7 Basi ilikuwa moyoni mwake Daudi, baba yangu, kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wa Israeli.
8 Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako;
9 lakini si wewe utakayeijenga nyumba hiyo; ila mwanao atakayetoka katika viuno vyako, yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu.