15 Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa.
16 Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.
17 Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;
18 ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.
19 Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;
20 ndipo nitawang’oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.
21 Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona BWANA ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?