16 Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.
17 Nawe, ukienda mbele yangu kama alivyokwenda Daudi baba yako, ufanye sawasawa na yote niliyokuamuru, na kuzishika sheria zangu na hukumu zangu;
18 ndipo nitakithibitisha kiti cha enzi cha ufalme wako, kama nilivyoagana na Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa kuwa na mtu wa kutawala katika Israeli.
19 Lakini mkigeuka, na kuziacha sheria zangu na amri zangu nilizoweka mbele yenu, mkienda, na kuitumikia miungu mingine, na kuiabudu;
20 ndipo nitawang’oa katika nchi yangu niliyowapa; na nyumba hii niliyoitakasa kwa jina langu, nitaiondosha itoke mbele zangu, nami nitaifanya kuwa mithali na tukano katikati ya watu wote.
21 Na nyumba hii, iliyo juu, kila apitaye ataona ushangao, atasema, Mbona BWANA ameitendea hivi nchi hii, na nyumba hii?
22 Nao watajibu, Kwa sababu walimwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu, na kuitumikia; kwa hiyo ameyaleta mabaya haya yote juu yao.