1 Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani, alikuja ili amjaribu Sulemani kwa maswali ya fumbo huko Yerusalemu, mwenye wafuasi wengi, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akamwambia mambo yote aliyokuwa nayo moyoni mwake.
2 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.
3 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,
4 na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia.
5 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6 Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.