11 Mfalme akayafanya kwa miti hiyo ya msandali madari ya nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haijatokea kama hiyo katika nchi ya Yuda.
12 Mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya vile alivyomletea mfalme. Basi akarudi, akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.
13 Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita za dhahabu;
14 mbali na ile waliyoileta wachuuzi na wafanya biashara; tena wafalme wote wa Arabuni, na maliwali wa nchi wakamletea Sulemani dhahabu na fedha.
15 Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; ngao moja hupata shekeli mia sita za dhahabu iliyofuliwa.
16 Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kigao kimoja hupata shekeli mia tatu za dhahabu; mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.
17 Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.