5 Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda.
6 Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.
7 Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!
8 BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.
10 Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu BWANA amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?
11 Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu BWANA ndiye aliyemwagiza.