2 Sam. 19:5-11 SUV

5 Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako;

6 kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako.

7 Basi sasa, ondoka, utoke nje, ukaseme na watumishi wako maneno ya kuwatuliza roho zao; maana mimi nakuapia kwa BWANA, usipotoka, hatabaki hata mtu mmoja pamoja nawe usiku huu; na mambo haya yatakuwa mabaya kwako kuliko mabaya yote yaliyokupata tokea ujana wako hata sasa.

8 Ndipo mfalme akaondoka, akaketi langoni. Nao wote wakaambiwa ya kwamba, Angalieni, mfalme ameketi langoni; watu wote wakaenda huko mbele ya mfalme.Basi, Israeli wote walikuwa wamekimbia kila mtu hemani kwake.

9 Wakashindana watu wote katika kabila zote za Israeli, wakisema, Mfalme alitutoa mikononi mwa adui zetu, akatuokoa mikononi mwa Wafilisti; naye sasa amekimbia kutoka nchi hii mbele ya Absalomu.

10 Na huyo Absalomu, tuliyemtia mafuta ili awe juu yetu, amekufa vitani. Basi sasa mbona ninyi hamsemi neno lo lote juu ya kumrudisha tena mfalme?

11 Naye mfalme Daudi akatuma kwa Sadoki na Abiathari, makuhani, kusema, Neneni na wazee wa Yuda, mkisema, Kwa nini ninyi mmekuwa wa mwisho wa kumrudisha tena mfalme nyumbani kwake? Kwa maana maneno ya Israeli wote yamemjia mfalme, ili kumleta nyumbani kwake.