2 Bwana MUNGU ameapa kwa utakatifu wake, ya kuwa, tazama, siku zitawajilia, watakapowaondoa ninyi kwa kulabu, na mabaki yenu kwa ndoana.
3 Nanyi mtatoka kwenye mahali palipobomolewa, kila mwanamke moja kwa moja mbele yake; nanyi mtajitupa katika Harmoni, asema BWANA.
4 Njoni Betheli, mkakose; njoni Gilgali, mkaongeze makosa; kaleteni dhabihu zenu kila asubuhi, na zaka zenu kila siku ya tatu;
5 mkachome sadaka ya shukrani, ya kitu kilichotiwa chachu; mkatangaze sadaka mtoazo kwa hiari na kuzihubiri habari zake; kwa maana ndivyo viwapendezavyo ninyi, enyi wana wa Israeli, asema Bwana MUNGU.
6 Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
7 Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika.
8 Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.