6 Mimi nami nimewapa usafi wa meno katika miji yenu yote, na kutindikiwa na mkate mahali penu pote; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
7 Tena nimeizuia mvua msiipate, ilipobaki miezi mitatu kabla ya mavuno; nami nimenyesha mvua juu ya mji mmoja, nikaizuia mvua isinyeshe juu ya mji mwingine; sehemu moja ilipata mvua, na sehemu isiyopata mvua ilikatika.
8 Basi kutoka miji miwili mitatu walitanga-tanga kuendea mji mwingine wapate kunywa maji, wasipate ya kuwatosha; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
9 Nami nimewapiga kwa ukavu na koga; wingi wa bustani zenu na mashamba yenu ya mizabibu, na mitini yenu na mizeituni yenu imeliwa na tunutu; Lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
10 Nimewapelekea tauni, kama tauni ya Misri; vijana wenu nimewaua kwa upanga, na farasi wenu nimewachukulia mbali; nami nimeupandisha uvundo wa matuo yenu na kuuingiza katika mianzi ya pua zenu; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
11 Baadhi yenu nimewaangamiza, kama hapo Mungu alipoiangamiza Sodoma na Gomora, nanyi mkawa kama kinga kilichonyakuliwa motoni; lakini hamkunirudia mimi, asema BWANA.
12 Basi nitakutenda hivi, Ee Israeli, na kwa sababu nitakutenda hivi, ujiweke tayari kuonana na Mungu wako, Ee Israeli.