5 Kwa maana Bwana, MUNGU wa majeshi, ndiye aigusaye nchi, nayo ikayeyuka, na wote wakaao ndani yake wataomboleza; nayo itainuka yote pia kama Mto, nayo itakupwa tena kama Mto wa Misri.
6 Yeye ndiye avijengaye vyumba vyake mbinguni, na kuweka misingi ya kuba yake juu ya nchi; yeye ndiye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; BWANA ndilo jina lake.
7 Je! Ninyi si kama wana wa Wakushi kwangu mimi, enyi wana wa Israeli, asema BWANA? Je! Mimi sikuwapandisha Israeli toka nchi ya Misri, na Wafilisti toka Kaftori, na Washami toka Kiri?
8 Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA.
9 Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini.
10 Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele.
11 Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;