8 Angalieni, macho ya Bwana MUNGU yanauangalia ufalme wenye dhambi, nami nitauangamiza utoke juu ya uso wa dunia; lakini sitaiangamiza kabisa nyumba ya Yakobo, asema BWANA.
9 Kwa maana, angalieni, nitatoa amri, nami nitaipepeta nyumba ya Israeli katika mataifa yote, kama vile ngano ipepetwavyo katika ungo lakini hata chembe moja iliyo ndogo haitaanguka chini.
10 Wenye dhambi wote katika watu wangu watakufa kwa upanga, hao wasemao, Mabaya hayatatupata nyuma wala mbele.
11 Siku hiyo nitaiinua tena maskani ya Daudi iliyoanguka, na kuziba mahali palipobomoka; nami nitayainua magofu yake, na kuyajenga kama siku za kale;
12 wapate kuyamiliki mabaki ya Edomu, na mataifa yote yaitwayo kwa jina langu, asema BWANA, afanyaye hayo.
13 Angalieni, siku zinakuja, asema BWANA, ambazo huyo alimaye atamfikilia avunaye, na yeye akanyagaye zabibu atamfikilia apandaye mbegu; nayo milima itadondoza divai tamu, na vilima vyote vitayeyuka.
14 Nami nitawarejeza tena watu wangu Israeli waliohamishwa, nao wataijenga miji iliyoachwa maganjo, na kukaa ndani yake; nao watapanda mizabibu katika mashamba, na kunywa divai yake; nao watafanyiza bustani, na kula matunda yake.