11 Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.)
12 Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe.
13 Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa.
14 Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo?
15 Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini.
16 Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao.
17 Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.