3 Baada yake huyo akainuka Yairi, Mgileadi; naye akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na miwili.
4 Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi.
5 Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni.
6 Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha BWANA, wala hawakumtumikia yeye.
7 Hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni.
8 Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng’ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane.
9 Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana.