15 Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba.
16 Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose.
17 Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni watu waume mia nne elfu, wenye kutumia upanga; hao wote walikuwa ni watu wa vita.
18 Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? BWANA akawaambia, Yuda atakwea kwanza.
19 Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao juu ya Gibea.
20 Watu wa Israeli walitoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea.
21 Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakaangamiza hata nchi watu ishirini na mbili elfu katika Israeli siku hiyo.