5 Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;
6 wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.
7 Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakamsahau BWANA, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.
8 Kwa hiyo hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.
9 Kisha wana wa Israeli walipomlingana BWANA, BWANA akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10 Roho ya BWANA ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye BWANA akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.
11 Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.