23 Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu;
24 ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze.
25 Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang’anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa.
26 Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye.
27 Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki.
28 Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani?
29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje.