27 Kwa sababu hiyo, Ee mfalme, shauri langu lipate kibali kwako; ukaache dhambi zako kwa kutenda haki, ukaache maovu yako kwa kuwahurumia maskini; huenda ukapata kuzidishiwa siku zako za kukaa raha.
28 Hayo yote yakampata mfalme Nebukadreza.
29 Baada ya miezi kumi na miwili, alikuwa akitembea ndani ya jumba la kifalme katika Babeli.
30 Mfalme akanena, akasema, Mji huu sio Babeli mkubwa nilioujenga mimi, uwe kao langu la kifalme, kwa uwezo wa nguvu zangu, ili uwe utukufu wa enzi yangu?
31 Hata neno lile lilipokuwa katika kinywa cha mfalme, sauti ilikuja kutoka mbinguni, ikisema, Ee mfalme Nebukadreza, maneno haya unaambiwa wewe; Ufalme huu umeondoka kwako.
32 Nawe utafukuzwa mbali na wanadamu, na makao yako yatakuwa pamoja na wanyama wa kondeni; utalishwa majani kama ng’ombe, na nyakati saba zitapita juu yako, hata utakapojua ya kuwa Aliye juu ndiye anayemiliki katika ufalme wa wanadamu, naye humpa amtakaye, awaye yote.
33 Saa iyo hiyo jambo hilo likatimizwa, likampata Nebukadreza; alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng’ombe, na mwili wake ulilowa maji kwa umande wa mbinguni, hata nywele zake zikakua, zikawa kama manyoya ya tai, na kucha zake kama kucha za ndege.