10 Kwa habari za mfano wa nyuso zao; walikuwa na uso wa mwanadamu; na hao wanne walikuwa na uso wa simba upande wa kuume; na hao wanne walikuwa na uso wa ng’ombe upande wa kushoto; na hao wanne walikuwa na uso wa tai pia.
11 Na nyuso zao na mabawa yao yalikuwa yametengana kwa juu; mabawa mawili ya kila mmoja yaliungana, hili na hili, na mawili yalifunika miili yao.
12 Nao walikwenda kuelekea mbele, kila mmoja wao; roho ilikotaka kwenda ndiko walikokwenda; hawakugeuka walipokwenda.
13 Kwa habari za kuonekana kwao vile viumbe hai; kuonekana kwao kulikuwa kama makaa ya moto yawakayo, kama kuonekana kwa vinga vya moto; moto ule ulikuwa ukienda juu na kushuka chini, katikati ya vile viumbe hai; na ule moto ulikuwa na mwangaza mwingi, na katika ule moto ulitoka umeme.
14 Na vile viumbe hai walipiga mbio, kwenda na kurudi, kama kuonekana kwa kumulika kwa umeme.
15 Basi, nilipokuwa nikivitazama vile viumbe hai, tazama, gurudumu moja juu ya nchi, karibu na kila kimoja cha vile viumbe hai, pande zake zote nne.
16 Kuonekana kwake magurudumu hayo na kazi yake kulikuwa kama rangi ya zabarajadi; nayo yote manne yalikuwa na mfano mmoja; na kuonekana kwake na kazi yake kulikuwa kana kwamba ni gurudumu ndani ya gurudumu lingine.