22 Tena juu ya vichwa vya viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa anga, kama rangi ya bilauri, lenye kutisha, limetandwa juu ya vichwa vyao.
23 Na chini ya anga mabawa yao yamenyoshwa, moja kulielekea la pili; kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande mmoja, na kila mmoja alikuwa na mawili yaliyowafunika miili yao upande wa pili.
24 Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.
25 Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao.
26 Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake.
27 Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote.
28 Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa BWANA. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mmoja anenaye.