1 Ndipo nikaangalia, na tazama, katika anga lililokuwa juu ya vichwa vya makerubi, kulionekana juu yao kana kwamba ni yakuti samawi, kuonekana kama mfano wa kiti cha enzi.
2 Naye akamwambia mtu yule aliyevaa bafta, akasema, Ingia kati ya magurudumu yazungukayo, yaani, chini ya kerubi, ukaijaze mikono yako yote miwili makaa ya moto, toka katikati ya makerubi, ukayamwage juu ya mji. Akaingia ndani mbele ya macho yangu.
3 Basi, makerubi walisimama upande wa kuume wa nyumba, hapo alipoingia mtu yule; nalo wingu likaujaza ua wa ndani.
4 Utukufu wa BWANA ukapaa kutoka kwa kerubi yule, ukasimama juu ya kizingiti cha nyumba; nayo nyumba ikajazwa na lile wingu, na ua ulikuwa umejaa mwangaza wa utukufu wa BWANA.
5 Na sauti ya mabawa ya makerubi ikasikiwa, hata katika ua wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi, asemapo.