1 Kisha neno la BWANA likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la BWANA;
3 Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!
4 Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali palipo ukiwa.
5 Hamkupanda kwenda mahali palipobomolewa, wala hamkuitengenezea nyumba ya Israeli boma, wapate kusimama vitani katika siku ya BWANA.
6 Wameona ubatili, na uganga wa uongo, hao wasemao, BWANA asema; lakini BWANA hakuwatuma; nao wamewatumainisha watu ya kuwa neno lile litatimizwa.
7 Je! Hamkuona maono ya bure, hamkunena mabashiri ya uongo? Nanyi mwasema, BWANA asema; ila mimi sikusema neno.