23 Tena naliwainulia mkono wangu jangwani, kwamba nitawatawanya kati ya mataifa, na kuwatapanya katika nchi mbalimbali;
24 kwa sababu hawakuzitekeleza hukumu zangu, bali walizikataa amri zangu, nao walizitia unajisi sabato zangu, na macho yao yaliandama vinyago vya baba zao.
25 Tena naliwapa amri zisizokuwa njema, na hukumu ambazo hawakuweza kuishi kwazo;
26 nami nikawatia unajisi kwa matoleo yao wenyewe, kwa kuwa walipitisha motoni wote waliofungua tumbo; ili kuwafanya kuwa ukiwa, wakapate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA.
27 Basi, mwanadamu, sema na nyumba ya Israeli, uwaambie, Bwana MUNGU asema hivi; Baba zenu wamenitukana kwa jambo hili, kwa kuwa wamekosa kosa juu yangu.
28 Kwa maana nilipokuwa nimekwisha kuwaingiza katika nchi ile, ambayo naliuinua mkono wangu kuwapa, wakati huo walipoona kila mlima mrefu, na kila mti wenye majani mengi, walitoa matoleo yao huko, na huko walitoa chukizo la sadaka zao, na huko walifanya nukato la kupendeza, na huko walimimina sadaka zao za kunywewa.
29 Ndipo nikawauliza, Nini maana yake mahali palipoinuka mnapopaendea? Basi, jina lake mahali pale ni Bama hata leo.