21 Naam, nitawakusanya, na kuwafukutia moto wa ghadhabu yangu, nanyi mtayeyushwa kati yake.
22 Kama fedha iyeyushwavyo kati ya tanuu, ndivyo mtakavyoyeyushwa kati yake; nanyi mtajua ya kuwa mimi, BWANA, nimemwaga ghadhabu yangu juu yenu.
23 Neno la BWANA likanijia, kusema,
24 Mwanadamu, uiambie nchi, Wewe u nchi isiyosafika, wala kunyeshewa mvua siku ya ghadhabu.
25 Fitina ya manabii wake imo ndani yake, kama simba angurumaye akirarua mawindo; wamekula roho za watu; hutwaa kwa nguvu hazina na vitu vya thamani; wameongeza hesabu ya wajane wake ndani yake.
26 Makuhani wake wameihalifu sheria yangu, wametia unajisi vitu vyangu vitakatifu; hawakuweka tofauti ya vitu vitakatifu na vitu vya kutumiwa sikuzote; wala hawakuwafundisha watu kupambanua vitu vichafu na vitu vilivyo safi, nao wamefumba macho yao, wasiziangalie sabato zangu, nami nimetiwa unajisi kati yao.
27 Wakuu wake kati yake wamekuwa kama mbwa-mwitu wakirarua mawindo; ili kumwaga damu, na kuharibu roho za watu, wapate faida kwa njia isiyo halali.