1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, Kwa sababu Tiro amesema juu ya Yerusalemu, Aha! Yeye amevunjika aliyekuwa lango la kabila za watu; amenigeukia; nitajazwa kwa kuwa sasa ameharibika;
3 basi Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, Ee Tiro, nami nitaleta mataifa mengi kupigana nawe, kama bahari iinuavyo mawimbi yake.
4 Nao wataziharibu kuta za Tiro, na kuibomoa minara yake; tena nitakwangua hata mavumbi yake yamtoke, na kumfanya kuwa jabali tupu.
5 Naye atakuwa mahali pa kutandazia nyavu za wavuvi kati ya bahari; maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana MUNGU; naye atakuwa mateka ya mataifa.
6 Na binti zake walio katika mashamba watauawa kwa upanga; nao watajua ya kuwa mimi ndimi BWANA.