10 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaukomesha wingi wa watu wa Misri, kwa mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli.
11 Yeye, na watu wake pamoja naye, watu wa mataifa watishao, wataletwa waingie katika nchi waiharibu, nao watafuta panga zao wapigane na Misri, na kuijaza nchi wale waliouawa.
12 Nami nitaikausha mito, na kuiuza nchi, na kuitia katika mikono ya watu wabaya; nami nitaifanya nchi kuwa ukiwa, na watu wote walio ndani yake, kwa mkono wa wageni; mimi, BWANA, nimenena neno hili.
13 Bwana MUNGU asema hivi; Pia nitaviharibu vinyago, nami nitavikomesha vitu vya ubatili katika Nofu, wala hapatakuwa na mkuu tena atokaye katika nchi ya Misri, nami nitatia hofu katika nchi ya Misri.
14 Nami nitaifanya Pathrosi kuwa ukiwa, nami nitatia moto katika Soani, nami nitatekeleza hukumu katika No.
15 Nami nitamwaga ghadhabu yangu juu ya Sini, ngome ya Misri, nami nitakatilia mbali wingi wa watu wa No.
16 Nami nitatia moto katika Misri; Sini itakuwa katika dhiki kuu, na No itavunjika kabisa; na Nofu itakuwa na adui wakati wa mchana.