1 Ikawa katika mwaka wa kumi na mmoja, mwezi wa tatu, siku ya kwanza ya mwezi, neno la BWANA likanijia, kusema,
2 Mwanadamu, mwambie Farao mfalme wa Misri, na jamii ya watu wake, Je! Umefanana na nani katika ukuu wako?
3 Tazama, Mwashuri alikuwa mwerezi katika Lebanoni, wenye matawi mazuri, na kifuniko chenye uvuli, na kimo kirefu; na kilele chake kilikuwa kati ya matawi mapana.
4 Maji yalimlisha, vilindi vilimsitawisha; mito yake ilipita pande zote za miche yake; naye akapeleka mifereji yake kwa miti yote ya kondeni.
5 Basi kimo chake kilitukuzwa kuliko miti yote ya kondeni, na vitanzu vyake viliongezeka; matawi yake yakawa marefu, kwa sababu ya maji mengi, alipoyachipuza.