16 Watu wote wa nchi watatoa toleo hili kwa ajili ya mkuu katika Israeli.
17 Tena itakuwa kazi ya mkuu kutoa hizo sadaka za kuteketezwa, na sadaka za unga, na sadaka za vinywaji, katika sikukuu, na katika mwezi mpya, na katika sabato, katika sikukuu zote za nyumba ya Israeli zilizoamriwa; atatengeneza sadaka ya dhambi, na sadaka ya unga, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ya Israeli.
18 Bwana MUNGU asema hivi; Mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, utatwaa ng’ombe mchanga mume mkamilifu; nawe utapatakasa mahali patakatifu.
19 Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani.
20 Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho.
21 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.
22 Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng’ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.