19 Na kuhani atatwaa baadhi ya damu ya sadaka ya dhambi, na kuitia juu ya miimo ya milango ya nyumba, na juu ya pembe nne za daraja ya madhabahu, na juu ya miimo ya lango la ua wa ndani.
20 Nawe utafanya vivyo hivyo katika mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi kwa ajili ya kila mtu akosaye, na kwa ajili ya mtu aliye mjinga, ndivyo mtakavyoifanyia nyumba upatanisho.
21 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, mtakuwa na Pasaka, sikukuu ya siku saba; mkate usiotiwa chachu utaliwa.
22 Na siku hiyo mkuu atatengeneza ng’ombe kuwa sadaka ya dhambi, kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu wote wa nchi.
23 Tena, katika zile siku saba za sikukuu atamtengenezea BWANA sadaka ya kuteketezwa, ng’ombe saba na kondoo waume saba wakamilifu, kila siku kwa muda wa siku saba, na beberu mmoja kila siku kuwa sadaka ya dhambi.
24 Naye atatengeneza sadaka ya unga, efa moja kwa ng’ombe, na efa moja kwa kondoo mume, na hini moja ya mafuta kwa efa moja;
25 katika mwezi wa saba, siku ya kumi na tano ya mwezi, katika sikukuu atafanya vivyo hivyo kwa muda wa siku saba; sadaka ya dhambi vivyo hivyo, na sadaka ya kuteketezwa vivyo hivyo, na sadaka ya unga vivyo hivyo, na mafuta vivyo hivyo.