1 Basi hapo Ezra alipokuwa akiomba na kuungama, akilia, na kujiangusha kifudifudi mbele ya nyumba ya Mungu, wakamkusanyikia katika Israeli wote kusanyiko kubwa sana la wanaume, na wanawake, na watoto; maana watu hao walikuwa wakilia sana.
2 Hata Shekania, mwana wa Yehieli, mmoja wa wana wa Elamu, akajibu, akamwambia Ezra, Sisi tumemkosa Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi; lakini kungaliko tumaini kwa Israeli katika jambo hili.
3 Haya basi! Na tufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu, na wale waliozaliwa nao, tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya na yatendeke kwa kuifuata torati.
4 Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.