3 Wakaiweka madhabahu juu ya msingi wake; maana hofu imewashika kwa sababu ya watu wa nchi; wakamtolea BWANA sadaka za kuteketezwa juu yake, sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni.
4 Wakaishika Sikukuu ya Vibanda, kama ilivyoandikwa, wakatoa sadaka za kuteketezwa za kila siku kwa hesabu yake, kama ilivyoagizwa, kama ilivyopasa kila siku;
5 na baadaye sadaka ya kuteketezwa ya daima, na za mwandamo wa mwezi, na za sikukuu za BWANA, zilizoamriwa na kuwekwa wakfu, na za kila mtu aliyemtolea BWANA sadaka kwa hiari yake.
6 Tangu siku ya kwanza ya mwezi wa saba walianza kumtolea BWANA sadaka za kuteketezwa, lakini msingi wa hekalu la BWANA ulikuwa haujawekwa bado.
7 Tena waliwapa waashi na maseremala fedha; wakawapa watu wa Sidoni, na watu wa Tiro, chakula, na vinywaji, na mafuta, ili walete mierezi kutoka Lebanoni mpaka Yafa kwa njia ya bahari, kwa kadiri walivyopewa ruhusa na Koreshi, mfalme wa Uajemi.
8 Hata mwaka wa pili wa kufika kwao nyumbani kwa Mungu, huko Yerusalemu, mwezi wa pili, Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, na ndugu zao wengine, makuhani na Walawi, na watu wote, waliotoka katika uhamisho na kufika Yerusalemu, wakaanza; nao wakawaweka Walawi, hao wenye miaka ishirini na waliozidi, ili kuisimamia kazi ya nyumba ya BWANA.
9 Ndipo wakasimama Yeshua, na wanawe na ndugu zake, Kadmieli, na wanawe, wana wa Hodavia, pamoja, ili kuwasimamia hao wafanyao kazi katika nyumba ya Mungu; wana wa Henadadi, pamoja na wana wao, na ndugu zao, Walawi.