14 Nao wazee wa Wayahudi wakajenga, wakafanikiwa, kwa msaada wa kuhubiri kwao Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido. Wakajenga, wakaimaliza kazi yao, kwa maagizo ya Mungu wa Israeli, na kwa amri ya Koreshi, na Dario, na Artashasta mfalme wa Uajemi.
15 Nyumba hiyo ikamalizika siku ya tatu ya mwezi Adari, katika mwaka wa sita wa kutawala kwake mfalme Dario.
16 Na wana wa Israeli, na makuhani na Walawi, na watu wengine katika hao waliohamishwa, wakaiweka wakfu nyumba ya Mungu kwa furaha.
17 Na katika kuiweka wakfu nyumba ya Mungu, wakatoa sadaka, ng’ombe mia, na kondoo waume mia mbili, na wana-kondoo mia nne; tena wakatoa mbuzi waume kumi na wawili, kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli wote, kwa hesabu ya kabila za Israeli.
18 Wakawaweka makuhani katika kura zao, wakawaweka na Walawi katika zamu zao, kwa ajili ya huduma ya Mungu, iliyokuwako Yerusalemu; vile vile kama vilivyoandikwa katika chuo cha Musa.
19 Kisha, wana wa uhamisho wakaifanya Pasaka, mwezi wa kwanza siku ya kumi na nne ya mwezi.
20 Kwa maana makuhani na Walawi walikuwa wamejitakasa wote pamoja; wote walikuwa hali ya tohara; wakachinja Pasaka kwa ajili ya wana wote wa uhamisho, na kwa ajili ya ndugu zao makuhani, na kwa ajili ya nafsi zao.