27 Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.
28 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.
29 Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake.
30 Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.
31 Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi.
32 Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote.
33 Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za BWANA ziliwaka juu ya watu, BWANA akawapiga watu kwa pigo kuu mno.