22 Tena mtakapokosa, msiyashike maagizo hayo yote BWANA aliyomwambia Musa,
23 hayo yote BWANA aliyowaagiza kwa mkono wa Musa, tangu siku hiyo BWANA aliyoleta maagizo, na baadaye katika vizazi vyenu
24 ndipo itakapokuwa, kama ni kosa lililofanywa pasipo kujua, wala mkutano haukuwa na fahamu, ndipo mkutano wote utasongeza ng’ombe mume mmoja mdogo kuwa sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA, pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji, kama amri ilivyo, na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi.
25 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mkutano wote wa wana wa Israeli, nao watasamehewa; maana, lilikuwa ni kosa, nao wamekwisha leta matoleo yao, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, na sadaka yao ya dhambi pia wameileta mbele za BWANA kwa ajili ya kosa lao;
26 nao mkutano wote wa wana wa Israeli watasamehewa, na mgeni akaaye kati yao; maana, katika habari za hao wote jambo hilo lilitendeka pasipo kujua.
27 Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi.
28 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za BWANA, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa.