36 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
37 Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu;
38 vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za BWANA, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli.
39 Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu;
40 viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za BWANA; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama BWANA alivyonena naye, kwa mkono wa Musa.
41 Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung’unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa BWANA.
42 Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa BWANA ukaonekana.