2 Hii ndiyo amri ya sheria BWANA aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng’ombe mke mwekundu asiye na kipaku, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado;
3 nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake;
4 kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba;
5 kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng’ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto;
6 kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng’ombe.
7 Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hata jioni.
8 Na huyo aliyemchoma moto ng’ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.