6 Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.
7 Akatunga mithali yake, akasema,Balaki amenileta kutoka Aramu,Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki,Njoo! Unilaanie Yakobo,Njoo! Unishutumie Israeli.
8 Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani?Nimshutumuje, yeye ambaye BWANA hakumshutumu?
9 Kutoka kilele cha majabali namwona;Na kutoka milimani namtazama;Angalia, ni watu wakaao peke yao,Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.
10 Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo,Au kuhesabu robo ya Israeli?Na nife kifo chake mwenye haki,Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.
11 Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa.
12 Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile BWANA atialo kinywani mwangu?