1 Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
2 Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema,
3 Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha BWANA katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume.
4 Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.