1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2 Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.
3 Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea BWANA; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.
4 Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;
5 pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.
6 Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.
7 Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia BWANA katika mahali hapo patakatifu.