12 ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama BWANA kwa moyo wote.
13 Na hasira za BWANA ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa BWANA kikaisha angamia.
14 Na tazama, ninyi mmeinuka badala ya baba zenu, maongeo ya watu wenye dhambi, ili kuongeza tena hizo hasira kali za BWANA juu ya Israeli.
15 Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote.
16 Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;
17 lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.
18 Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.